Wednesday, January 14, 2015

Kauli ya Waziri Chikawe kuhusiana na Waganga wanaochangia mauaji ya Albino

albinoMatukio ya kuuawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Albino’ bado yameonekana kuendelea kuchukua nafasi hasa katika Mikoa ya kanda ya Ziwa hali inayozidi kutishia amani ndani ya familia nyingi.
Waziri wa mambo ya ndani Mathias Chikawe ametoa tamko kuwa kutakua na operesheni ya kitaifa ya kuwasaka na kuwakamata waganga wa kienyeji maarufu kama wapiga ramli  ili kuwafikisha mahakamani.
byUamuzi wa Waziri huyo unatokana na kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa watu wenye ulemavu vikishika kazi kutokana na kuuawa kwa imani za kishirikina.
Chikawe alisema watashirikiana na Chama cha watu wenye ulemavu TAS kuwabaini wahalifu na kuwachukulia hatua ili kupunguza vitendo hivyo.

PROF. MARK MWANDOSYA AFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI SUDANI

New Picture (1)
Mhe. Prof. Mark Mwandosya akifafanua jambo wakati wa mkutano wa pamoja na Waziri wa Maji na Umeme wa Sudan Mhe Mutaz Moussa Abdallah Salim. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bwana Felix Ngamlagosi ambaye ameongozana pamoja na maafisa wengine na Waziri Prof. Mwandosya
New Picture (2)
Mhe. Prof. Mark Mwandosya akitoa maelezo katika mkutano wa pamoja na Waziri wa Maji na Umeme wa Sudan Mhe Mutaz Moussa Abdallah Salim.
New Picture (3)
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Mhe. Prof. Mark Mwandosya katika mkutano wa pamoja na ujumbe wa Sudan ulioongozwa na Waziri wa Maji na Umeme wa Sudan Mhe Mutaz Moussa Abdallah Salim.
New Picture
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Mhe. Prof. Mark Mwandosya akikaribishwa na mwenyeji wake Waziri wa Maji na Umeme wa Sudan Mhe. Mutaz Moussa Abdallah Salim mara alipowasili katika Ofisi za Wizara hiyo Jijini Khartoum.
12 – 17 JANUARI 2015
Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya yuko ziarani nchini Sudan ambako atatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo nchini humo ikiwemo miradi mikubwa ya mabwawa yaliyojengwa katika bonde la Mto Nile pamoja na kubadilishana uzoefu na taasisi za Sudan zinazojihusisha na udhibiti wa huduma katika sekta za maji, nishati, mawasiliano na usafirishaji.
Ujumbe wa Mhe. Prof. Mwandosya umejumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA).
Mhe. Prof. Mwandosya alianza ziara yake Jumatatu ya tarehe 12 Januari, 2015 kwa kutembelea Wizara ya Rasilimali za Maji na Nishati ya Umeme ya Jamhuri ya Sudan.
Katika ziara hiyo Mhe. Prof. Mwandosya alieleza kuwa pamoja na shughuli zingine, ameandamana na taasisi za udhibiti kutoka Tanzania ili kujifunza na kubalishana uzoefu katika shughuli za udhibiti kutoka kwa taasisi kama hizo katika nchi ya Sudan. Waziri alieleza kuwa shughuli za udhibiti Tanzania zimekuwa zikifanyika kwa kipindi cha takribani miaka 10 sasa. Waziri alieleza kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatika katika kutekeleza majukumu yao, Mamlaka za Udhibiti bado zina changamoto nyingi ambazo inabidi kukabiliana nazo kwa kujifunza na kubadilisha uzoefu na taasisi kama hizo katika nchi kama Sudan.

MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM

Mnyika naye amvalia njuga Prof. Muhongo


Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amemkalia kooni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akieleza kuwa endapo Rais Jakaya Kikwete hatamwajibisha, anakusudia kupeleka hoja bungeni ya kushughulikia uongo, udhaifu na utendaji mbovu katika wizara hiyo.

Mnyika , anakuwa mbunge wa pili kuahidi kutumia Bunge kumng’oa Mhongo akitanguliwa na mbunge wa Simanjiro (CCM) Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, aliyesema endapo Rais hatamuwajibisha atapaleka hoja binafsi bungeni ya kutokuwa na imani na viongozi hao.

Sendeka alisema hayo juzi katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wachimbaji wadogo na wamiliki wa migodi, uliofanyika mjini Mererani.

Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana, Mnyika alisema kuwa, kiporo cha Kikwete kuhusu Muhongo kinaendelea kuleta athari ndani ya wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapo tuhuma za kujipendelea kwenye uteuzi wa viongozi wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya wizara hiyo.

Mbunge huyo alisema anazo taarifa za ndani za wizara kuwa Shirika la Umeme (Tanesco), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Taasisi ya Uchunguzi wa Madini (MRI) kutumika kuficha udhaifu na ufisadi ukiwamo uteuzi wa watendaji.

Alisema zipo tuhuma mbalimbali alizipata kuhusu teuzi zilizofanywa kabla na baada ya kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow , ambako zaidi ya Shilingi bilioni 300 zilichotwa na kusababisha taharuki na chuki.

Alisema anakusudia kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge kupata ushahidi wa uteuzi uliofanyika.

“Kabla ya uteuzi huo, Profesa Muhongo alitangaza kwamba timu za wataalamu zimeundwa kuchambua mabadiliko ya muundo wa Tanesco, TPDC na MRI na kufanya uteuzi wa watendaji kwa ushindani.

Mnyika alisema kuna tuhuma za upendeleo katika mashirika na taasisi hizo zote tatu za wizara hiyo.

“Nitatoa kauli na kuchukua hatua baada ya kupata maelezo na vielelezo vyote kupitia vikao vya kamati za bunge hilo vinavyoanza kesho na mkutano wa Bunge unaotarajia kuanza Januari 27, mwaka huu,” alisema na kuongeza:

Wakati Mnyika akiyasema hayo, yapo madai kuwa, wajumbe wa bodi ya Tanesco iliyoteuliwa wiki iliyopita ina wajumbe wengi kutoka ukanda mmoja wa Tanzania.

Wajumbe wa bodi hiyo iliyoteuliwa na Profesa Muhongo ni Kissa Kilindu, Juma Mkobya, Dk. Haji Semboja, Shabaan Kayungilo, Dk. Mutesigwa Maingu, Boniface Muhegi, Felix Kibodya na Dk. Nyamajeje Weggoro.

Kadhalika kuna madai ya kuteuliwa kwa Mkurugenzi wa taasisi moja ya wizara kwa upendeleo akitoka kanda hiyo.

Kutokana na madai hayo, NIPASHE ilimtafuta Naibu Waziri, Charles Kitwanga, ambaye alishangaa Watanzania kuhoji ukabila badala ya vigezo walivyonavyo wateule hao.

“Karne ya 21 bado tunahoji ukabila, nilitegemea watu wangeuliza watu hawa waliopewa nafasi hizi wanavigezo gani, wengine hapa wameingia kwa vyeo vyao,” alisema.

CCM LINDI YAKUTANA KUWEKA MIKAKATI MIZURI

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa Ndugu Nape Nnauye akitoa salaam za pongezi kwa wananchi wa kijiji cha Kilangala B kata ya Kilangala  kwa kuipa ushindi CCM kwenye uchaguzi serikaliza mitaa uliofanyika desemba 2014, Katika mkutano huo Nape aliwaeleza wananchi hao CCM ndio chama pekee kinachotoa majibu kwa matatizo ya wananchi.

 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akiwa na Mwenyekiti  aliyeshinda uchaguzi Hamid Rashid Namtonda akitoa salaam za kushukuru wakazi wa kijiji cha Kilangala B kata ya Kilangala jimbo la Mchinga.
 Mwenyekiti wa kijiji cha Kilangala B akiwashukuru wananchi wake kwa kumchagua kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ,vijiji na vitongoji uliofanyika desemba 2014.
 Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mheshimiwa Said Mtanda akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Kilangala B wakati wa kumtano wa kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa kijiji hicho kuichagua CCM, mkutano huu ulifanyika tarehe 11 Januari 2015.
 Wananchi wakisikiliza salaam za shukrani kutoka kwa Viongozi wao.

 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akiwasalimu Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Lindi.
 Mbunge wa Jimbo la Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje Mheshimiwa Bernard Membe akiwasalimu wajumbe waliohudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Lindi.
MNEC wa Wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete akishauriana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Mwantumu Mahiza wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Lindi
Sehemu ya wajumbe waliohudhuria Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Lind

MAFINGA KUMECHANGAMKA

Kila mtu akiwa na harakati zake za kujiongezea kipato huku wengine wakisubiri usafiri. Hali ya hewa ni shwari kabisa.
      

CCM YAITAKA SERIKALI KUENDELEA KUTEKELEZA MAADHIMIO YA BUNGE

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi akizungungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Sekretarieti Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alipokuwa anazungumzia maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kilichofanyika Zanzibar tarehe 13 Januari 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Jana tarehe 13/01/2015 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake wa Taifa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ilifanya kikao chake cha kawaida cha siku moja Kisiwandui Mjini Zanzibar.

Pamoja na mambo mengine baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na Kamati Kuu ni pamoja na:-

1. SAKATA  LA  AKAUNTI  YA ESCROW
Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa sana na sakata hili. Baada ya kulijadili kwa muda mrefu na kwa kina Kamati Kuu imeamua yafuatayo:-,
i). Pamoja na yale ambayo yameshatekelezwa na serikali, Kamati Kuu imeitaka serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea kutekeleza maazimio ya bunge juu ya swala hilo.

ii). Kamati Kuu imewataka wote wanaopewa dhamana wajenge utamaduni wa kuwajibika kwa dhamana zao, na wasipowajibika waliowapa dhamana wachukue hatua za kuwawajibisha.

iii). Aidha Kamati Kuu imeiagiza Kamati Ndogo ya Maadili kuchukua hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili kwenye sakata la Escrow na wako kwenye vikao vya maamuzi vya Chama. Kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kitafanyika tarehe 19/01/2015 kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo.

2. WALIOPEWA  ADHABU KWA KUKIUKA MAADILI YA CHAMA.
Itakumbukwa kuna makada sita wa CCM walipewa adhabu kwa kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea urais, watamaliza muda wa adhabu zao mwezi wa pili mwaka 2015.

Baada ya muda wa adhabu zao kuisha, itafanyika tathimini kuona kama walizingatia mashariti ya adhabu zao. Na kama kuna ambao watakutwa hawakuzingatia mashariti ya adhabu zao wataongezewa adhabu.

3. SOKO LA MAHINDI
Kamati Kuu imepokea taarifa ya mwenendo wa soko la mahindi nchini. Baada ya tathimini na uchambuzi,  pamoja na kazi iliyofanywa na serikali, Kamati Kuu imeiagiza serikali kuangalia upya mfumo unaotumiwa na Hifadhi ya Taifa ya Chakula ( NFRA)katika ununuzi wa mahindi, ili unufaishe zaidi wakulima badala ya utaratibu wa sasa ambao kwa kiasi kikubwa unanufaisha zaidi mawakala badala ya wakulima moja kwa moja.

4. RATIBA YA VIKAO VYA CHAMA.
Kamati Kuu imepitisha ratiba ya shughuli mbalimbali za Chama kwa mwaka 2015.
Aidha ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM ndani ya dola utapangwa na vikao vijavyo  vya Chama

kamati kuu ya ccm jana zanzibar

 Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana mara baada ya kuwasili kwenye Afisi Kuu ya CCM Zanzibar tayari kwa kikao cha  Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
 Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Mrisho Kikwete   akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai leo alipofika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja  akihudhuria Kikao cha kawaida cha Kamati Kuu ya CCM Taifa(katikati) Katibu Mkuu wa CCM Taifa Abdulrahman Kinana . 
 
 Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akibadilishana mawazo na Katibu Mkuu wa CCM Taifa Abdulrahman Kinana katika viwanja vya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja leo walipohudhuria katika Kikao cha kawaida cha siku moja cha Kamati Kuu ya CCM Taifa. 


 Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akisalimiana na Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa Haji Mkema mara alipowasili Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja leo alipohudhuria katika Kikao cha kawaida cha siku moja cha Kamati Kuu ya CCM Taifa (wa pili kulia) Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai na  Katibu Mkuu wa CCM Taifa Abdulrahman Kinana (kushoto). 
 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai akisalimiana na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia Mjumbe wa Kamti Kuu ya CCM Taifa Dk.Mohammed Gharib Bilali wakati alipowasili Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja leo katika Kikao cha kawaida cha Kamati Kuu ya CCM Taifa chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Mrisho Kikwete. 



Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) akiongoza Kikao cha Kamati Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika leo katika ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja,

Mvua yaleta maafa Msumbiji



Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Msumbiji zimesababisha maafa makubwa ambapo watu kadhaa wamefariki na wengine kupoteza makazi yao.Serikali ya Msumbiji imetoa tahadhari ya hali ya juu kwenye eneo la kaskazini na katikati mwa nchi hiyo kufuatia mafuriko yaliyotokana na mvua hizo.Hadi sasa watoto 18 hawajuliani walipo na kuna taarifa watu kadhaa wamesombwa na maji yaliyokuwa yakitiririka katika mto mmoja.Mawasiliano ya barabara inayounganisha eneo la kati na kaskazini mwa nchi hiyo yameharibika.

RIPOTI KAMILI YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM KUJULIKANA LEO

Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akizungumza jambo na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM,Ndugu Adam Kimbisa,wakati akitoka nje mara baada ya kumaliza kikao cha kawaida cha Kamati Kuu ya CCM Taifa usiku huu,kilichofanyika jana katika ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Unguja,Zanzibar,kikao hicho kilianza mnamo majira ya saa sita mchana na kumalizika usiku mnamo saa mbili na ushehe hivi huku mambo mbalimbali yakiwa yamejadiliwa ikiwemo suala la sakata la Akaunti ya Escrow,Hali ya kisiasa nchini,uchaguzi Mkuu na mambo ya Maadili na mengineyo.
Pichani ni Katibu wa NEC-Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na Wanahabari usiku wa kuamkia leo baada ya kikao cha kamati kuu cha CCM kuisha nje ya ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM,Kisiwandui mjini Unguja kisiwani Zanzibar.Nape ameeleza kuwa taarifa rasmi ya yaliyohusu kikao hicho atayaweka wazi mapema leo asubuhi.

MAGAZETI LEO JUMATANO