Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imetoa siku 80 kwa uongozi wa Chama
cha Tanzania Labour (TLP) kuhakikisha kinafanya uchaguzi wake wa ndani
wa kuwapata viongozi wapya.
Kauli
hiyo imeitolewa baada ya baadhi ya wanachama wa chama hicho kufikisha
malalamiko katika ofisi hiyo wakiiomba itangaze kwamba uongozi wa
Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema umefikia kikomo.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ukweli na Maridhiano wa TLP Taifa, Joram Kinanda
alimtuhumu Mrema kukiuka katiba ya chama hicho, kuongoza chama
kidikteta, kuporomosha heshima ya chama na kujilimbikizia madaraka.
Akizungumza
ofisini kwake, Dar es Salaam jana, Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya
Siasa, Sisty Nyahoza alisema baada ya kusikiliza pande zote zinazosigana
ofisi hiyo iliwataka viongozi kuandaa uchaguzi.
"Tuliwasikiliza
wote upande wa Kinanda na upande wa Mrema ambaye alikuwa na sababu
kwamba alishindwa kuitisha uchaguzi kutokana na hali yake ya afya lakini
tumewaandikia barua kuwa ifikapo Aprili 26 wawe wamekwisha kufanya
uchaguzi na si vinginevyo," alisema Nyahoza na kuongeza: "Vyama hivi ili
viweze kujinasua na migogoro ya mara kwa mara lazima vijiendeshe kama
taasisi na si chama cha mtu mmoja. Hii itasaidia kukuza demokrasia
nchini na siku zote demokrasia inaanzia katika vyama vyetu ndipo inakuja
juu. kama vyama havina demokrasia ni ngumu hata huku juu kuwapo."
Malalamiko
ya Kinanda yalitolewa pia na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho,
Jeremiah Shelukindo aliposema jana kuwa aliamua kuandika barua ya
kujiuzulu tangu Desemba 15 mwaka jana kutokana na kutoridhishwa na
uongozi wa Mrema. Akizungumzia uamuzi huo Mrema alisema: "Kwanza
tunaishukuru Ofisi ya Msajili kwani ilielewa sababu tulizozitoa za
kutofanya uchaguzi, katiba yetu inaturuhusu kufanya hivyo na
tutatekeleza agizo hilo.
"Ofisi ya
Msajili ilituhakikishia lazima tufanye uchaguzi kamati kuu yetu
imekubaliana kwamba uchaguzi utafanyika Aprili 26 na maandalizi ya
uchaguzi huo yanakwenda vizuri."
Mrema
ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo akizungumzia tuhuma za Shelukindo alisema,
"Hazina ukweli wowote na tunaendesha chama kwa kuzingatia Katiba na
kanuni za chama na hao wanaosema mimi ni dikteta, hakuna jambo kama
hilo.
Vyama vinne vyasajiliwa
Katika
hatua nyingine, ikiwa imebaki miezi minane kabla ya kufanyika kwa
Uchaguzi Mkuu, vyama vinne vya siasa vimewasilisha barua ya maombi ya
usajili katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, huku vingine viwili
vikipatiwa usajili wa muda.
Vyama
vilivyopata usajili wa muda ni; Chama cha Wananchi na Demokrasia
(Chawade) kilichoasisiwa na Shabiri Mpaka na Pilly Athuman na Chama cha
Maridhiano na Uwiano (CMU) chini ya waasisi Jamali Abdallah na Shaibu
Hemed Likwimbi.
Chama cha
Kijamii na Uzalendo Tanzania (CKUT), chini ya waasisi wake Ramadhan
Semtawa na Noel Antapa kiliwasilisha maombi yake Januari 6. Vingine
vilivyowasilisha barua ya maombi tangu mwaka jana ni; Chama cha
Demokrasia na Umoja (Dau) ambacho waasisi ni Idd Mwishwa na Lazaro
Mwalusamba, Restoration of the National (RNP) chini ya waasisi Atis
Jacob Atto na Jenesta Josia na True Conscious for Liberation (TRUCOLI)
ambacho kimeasisiwa Leonard Nyongani na Boniface Magesa.CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment