Shem Ibrahim Karenga enzi za uhai wake.
MWANAMUZIKI mkongwe mwenye umahiri wa kuimba na kucharaza gitaa kiongozi la Solo, Shem Ibrahim Karenga amefariki dunia leo akiwa katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitibiwa.
Wengi wanamfahamu Shem Karenga kupitia tungo zake mbalimbali zilizochangia kumpa umarufu, alizozifyatua akiwa na bendi hizi na zile, kama vile ‘Tucheze Segere’, ‘Muna’, ‘Kila jambo’ na ‘Mbelaombe’.
HISTORIA YAKE KWA KIFUPI
Shem Karenga alizaliwa mwaka 1950, Bangwe, Kigoma na kupata elimu ya msingi katika shule ya kimishionari ya Kihezya kuanzia mwaka 1957 hadi mwaka 1964.
Mwaka 1964 alijiunga na bendi ya Lake Tanganyika Jazz ambayo maskani yake yalikuwa mjini Kigoma.
Mwaka 1972, aliitwa kwenye bendi ya Tabora Jazz kama mwanamuziki mwenye kipaji cha utunzi, mwimbaji na mpigaji wa gitaa la Solo.
Mwaka 1983 alijiengua kutoka Tabora Jazz na kusimama kabisa kujihusisha na muziki, ambako kilichofuatia ilikuwa ni kifo cha bendi hiyo.
Mwaka 1990 aliondoka Tabora na kutua jijini Dar es Salaam.
Mwaka 1990 alijiunga na MK Beats.
Mwaka 1995, MK Beats ilisambaratika, ambako mwaka uliofuata, yaani 1996 alianzisha bendi ya Tabora Jazz Star kwa kushirikiana na Ibrahim Didi.
Mpaka mauti yanamfika, Shem Karenga Mkurugenzi Msaidizi katika Bendi ya Tabora Jazz Star ambapo Mkurugenzi Mkuu ni Ibrahim Didi.
Kwa mujibu wa familia ya marehemu, Shem Karenga anatarajiwa kuzikwa kesho.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI, AMEN
No comments:
Post a Comment