Dar es
Salaam. Panga pangua ya saba ya Baraza la Mawaziri iliyofanyika juzi
imefikisha mawaziri 61 waliotemwa, kujiuzulu au kufariki dunia tangu
Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, huku mawaziri 16
wakihimili mawimbi hayo hadi sasa.
Katika
mabadiliko hayo saba yaliyofanywa katika kipindi cha miaka tisa, wako
waliobadilishwa wizara, kupandishwa kutoka naibu waziri kuwa waziri
kamili, huku sura mpya zikiingizwa.
Mabadiliko
hayo yalitokana na mawaziri kutakiwa kuwajibika kutokana na kashfa
mbalimbali, huku mengine yakitokana mawaziri kufariki na moja likitokana
na Waziri Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa.
Katika
panga pangua hiyo, mawaziri 16 wamefanikiwa kudumu katika baraza hilo
tangu Rais Kikwete aingie madarakani ambao ni Sofia Simba, Profesa Mark
Mwandosya, Stephen Wasira, Dk Hussein Mwinyi na Dk John Magufuli.
Wengine
ni Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia, Dk Mary
Nagu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye kabla ya kuteuliwa kushika
nafasi hiyo, alikuwa naibu waziri na baadaye waziri wa Tamisemi.
Mawaziri
wengine waliopo sasa ambao mwaka 2005 walikuwa manaibu mawaziri ni
Gaudencia Kabaka, Bernard Membe, Celina Kombani, Christopher Chiza na
Mathias Chikawe.
Naibu
waziri pekee ambaye alikuwamo katika baraza la mawaziri la kwanza la
Rais Kikwete akiwa na wadhifa huohuo ni Dk Makongoro Mahanga ambaye sasa
ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira.CHANZO:MWANANCHI
Waliotemwa
Mawaziri
waliotemwa au kujiuzulu tangu Rais Kikwete aingie madarakani, wakiwamo
wale walioshindwa katika kinyang'anyiro cha ubunge ni Edward Lowassa,
ambaye alijiuzulu, Antony Diallo, Dk Ibrahim Msabaha, Basil Mramba, John
Chiligati, Andrew Chenge, Joseph Mungai, Dk Emmanuel Nchimbi, Lawrence
Masha, Mustafa Mkulo, William Ngeleja, Dk Cyril Chami, Omary Nundu,
Bakari Mwapachu na Kingunge Ngoimbale-Mwiru.
Wengine
ni Ezekiel Maige, Dk Hadji Mponda, Teresa Huvisa, Shamsi Vuai Nahodha,
Nazir Karamagi, Dk Mathayo David, Khamis Kagasheki, Profesa Anna
Tibaijuka, Profesa Sospeter Muhongo, Dk Batilda Buriani, Joseph Mungai,
Diodorus Kamala, Mohamed Seif Khatib, Mwantumu Mahiza, Profesa Peter
Msola na Profesa David Mwakyusa, Philip Marmo na Juma Ngasongwa.
Naibu
mawaziri ni Dk Luca Siyame, Balozi Seif Ally Idd, Hezekiah Chibulunje,
Shamsa Mwangunga, Daniel Nsanzugwanko, Hezekiah Chibulunje, Rita Mlaki,
Dk Charles Mlingwa, Zabein Mhita, Athuman Mfutakamba, Dk Lucy Nkya,
Goodluck Ole Medeye, Benedict Ole Nangoro, Gregory Teu, Philipo Mulugo,
Mohamed Abood, Dk Aisha Kigoda, Omari Yusuf Mzee, Jeremiah Sumari, Dk
Maua Daftari, Zakia Meghji, Joel Bendera, Abdisalaam Issa Khatib na
James Wanyancha.Pia, wapo ambao walifariki dunia ambao ni Salome Mbatia,
Juma Akukweti, Jeremiah Sumari na William Mgimwa.
Badiliko la Kwanza
Katika
baraza lake la kwanza Rais Kikwete aliteua mawaziri na naibu mawaziri 60
Januari 2006 na ilipofika Oktoba 2006, Rais Kikwete alifanya mabadiliko
ya kwanza makubwa ya baraza lake la mawaziri kwa kuwahamisha vituo vya
kazi mawaziri 10 na naibu mawaziri wanane.
Mawaziri
waliohusika na mabadiliko hayo ni Diallo (Maliasili na Utalii) ambaye
alihamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Profesa Maghembe (Kazi,
Ajira na Maendeleo ya Vijana) kupelekwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dk
Msabaha (Nishati na Madini) alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Karamagi (Viwanda na Biashara) alihamishiwa Wizara ya
Nishati na Madini, Mramba (Miundombinu) alihamishiwa Viwanda na Biashara
na Chiligati (Mambo ya Ndani) alihamishiwa Wizara Kazi, Ajira na
Vijana.
Mawaziri
wengine ni Chenge (Ushirikiano Afrika Mashariki) alihamishiwa Wizara ya
Miundombinu, Dk Kawambwa (Maendeleo ya Mifugo) alihamishiwa Wizara ya
Maji, Wasira (Maji) alihamishiwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
na Mungai (Kilimo, Chakula na Ushirika) alihamishiwa Wizara ya Mambo ya
Ndani.
Naibu
Mawaziri waliohamishwa wizara zao na kupelekwa wizara nyingine ni Dk
Nchimbi (Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni) kwenda Wizara ya Kazi,
Nsanzugwanko (Kazi na Ajira) kwenda Wizara ya Habari, Michezo na
Utamaduni, Dk Mathayo (Biashara na Viwanda) kwenda Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika na Chibulunje (Kilimo, Chakula na Ushirika) kwenda
Wizara ya Viwanda na Biashara.
Wengine
ni Dk Buriani (Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto)
kuhamishiwa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Mbatia (Mipango,
Uchumi na Uwezeshaji) kwenda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto, Masha (Nishati na Madini) kwenda Mambo ya Ndani na Membe (Mambo
ya Ndani) kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Badiliko la Pili
Februari
2007, Rais Kikwete alifanya uteuzi wa mawaziri wawili na naibu waziri
wawili baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa. Nafasi ya Migiro ilichukuliwa na Membe.Dk Buriani
aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu)
kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha Akukweti. Kabla ya
uteuzi huo Buriani alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mipango, Uchumi na
Uwekezaji.
William
Ngeleja aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Gaudence
Kayombo aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwekezaji.
Badiliko la tatu
Februari
12, 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu
kutokana na kashfa ya Richmond, Kikwete alivunja Baraza la Mawaziri na
kuliunda upya.
Lowassa
alijiuzulu sambamba na waliokuwa mawaziri wawili Dk Msabaha na Karamagi
ambao wote walikuwa wameiongoza Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati
tofauti. Nafasi zao zilizibwa na William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk
Kamala (Afrika Mashariki), huku Pinda akiteuliwa kuchukua nafasi ya
Lowassa.
Badiliko la nne
Rais
Kikwete alifanya mabadiliko mara ya nne katika baraza lake Mei, 2008
baada ya Chenge, ambaye ni mbunge wa Bariadi, kujiuzulu kutokana na
kashfa ya ununuzi wa rada na nafasi yake kujazwa na mbunge wa Bagamoyo,
Dk Kawambwa huku Rais Kikwete pia akibadilisha mawaziri kadhaa.
Badiliko la tano
Mei 2012,
Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya tano katika baraza lake baada ya
kuwaondoa mawaziri sita baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu
za Serikali (CAG) kubaini kuwa walikiuka maadili ya utumishi wa umma na
kushindwa kuwajibika kisiasa kusimamia mali za umma.Katika mabadiliko
hayo waliondolewa walikuwa ni Mkulo (Fedha), Ngeleja (Nishati na
Madini), Dk Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Maige (Maliasili na
Utalii), Nundu (Uchukuzi) na Dk Chami (Viwanda na Biashara). Wengine
waliotemwa ni Mfutakamba (Naibu, Uchukuzi) na Naibu Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk Nkya.
Mawaziri
walioziba nafasi hizo ni William Mgimwa (Fedha), Kagasheki (Utalii), Dk
Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara),
Dk Mwinyi (Afya), Profesa Muhongo (Nishati na Madini), Dk Seif Rashid
(Naibu, Afya) na George Simbachawene (Naibu, Nishati na Madini).
Manaibu
wapya walioingia ni January Makamba (Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia), Dk Charles Tizeba (Uchukuzi) na Amos Makala (Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo). Wengine ni Dk Binilith Mahenge (Maji),
Stephen Masele (Nishati na Madini), Angela Kairuki (Katiba na Sheria),
Janet Mbene na Saada Mkuya Salum (Fedha).
Badiliko la sita
Januari
19, 2014, Rais Kikwete alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa
kuteua mawaziri wapya wawili na manaibu mawaziri wapya wanane, huku
akiwapandisha vyeo manaibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili.
Katika
mabadiliko hayo, Rais Kikwete aliwapumzisha Dk Terezya Huvisa, ambaye
alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Gregory Teu,
aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na Philipo Mulugo
aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wengine
waliopumzishwa ni Benedict Ole-Nangoro aliyekuwa naibu waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Goodluck Ole-Medeye aliyekuwa naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mabadiliko
hayo yalikuwa yanalenga kujaza nafasi zilizoachwa na Balozi Khamis
Kagasheki (Maliasili na Utalii, Dk Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi),
Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk Mathayo (Maendeleo ya
Mifugo) waliotemwa Desemba 2013 kutokana na kashfa ya Operesheni
Tokomeza na nafasi ya Dk Mgimwa, aliyefariki dunia kutokana na maradhi.
Mawaziri
wapya walioteuliwa wakati huo ni Dk Asha-Rose Migiro (Katiba na Sheria),
Dk Titus Kamani kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Wengine
aliowateua kuwa naibu mawaziri ni Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa
Fedha, Dk Kebwe Stephen, Naibu Waziri, Afya na Ustawi wa Jamii na
Jenista Mhagama, naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Pia, Dk
Pindi Chana aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto na Kaika Telele, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Wengine ni Godfrey Zambi, naibu Waziri Kilimo, Chakula na Ushirika,
Juma Nkamia, Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na
Mahmoud Mgimwa, Naibu Waziri, Maliasili na Utalii.Naibu mawaziri
waliopandishwa kuwa mawaziri ni Saada Mkuya (Waziri wa Fedha), Lazaro
Nyalandu (Maliasili na Utalii) na Dk Seif Seleman Rashidi ( Afya na
Ustawi wa Jamii), Dk Binilith Mahenge alipandishwa kutoka Naibu Waziri
wa Maji na kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).
Dk
Hussein Ali Mwinyi alihamishwa kutoka Afya na Ustawi wa Jamii kwenda
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na wengine kadhaa walihamishwa.
Badiliko la saba
Juzi,
Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya saba ambayo yanawezekana kuwa
yatakuwa ya mwisho kutokana na kusalia miezi sita kabla ya kuvunjwa kwa
Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.
Mabadiliko
hayo baada ya mawaziri wawili, Profesa Tibaijuka (kufutwa kazi) na
Profesa Sospeter kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Tegeta
Escrow.
Walioingia
ni manaibu waziri wawili, Charles Mwijage (Nishati na Madini) na Anna
Malecela (Elimu na Ufundi). Wengine walihamishwa ambao ni Wasira kutoka
Ofisi ya Rais kwenye Kilimo na Ushirika, Lukuvi kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu kwenda Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wengine ni Dk Nagu kwenda Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) na Jenister Mhagama (Waziri Mkuu, Uhusiano, Uratibu na Bunge).
Dk
Harrison Mwakyembe anahamia Afrika Mashariki (kutoka Uchukuzi) na nafasi
yake inachukuliwa na Sitta akitokea Wizara ya Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment