Sunday, January 25, 2015

Mnyika awasilisha hoja kupinga kura ya maoni

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amewasilisha taarifa kwa Katibu wa Bunge akitaka Bunge lijadili udhaifu wa katiba inayopendekezwa na kupitisha azimio la kuahirishwa kufanyika kwa kura ya maoni ya wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa katiba hiyo.

Pia amemtaka Rais Jakaya Kikwete kutangaza kufuta tangazo la serikali la kufanyika kwa kura hiyo mwishoni mwa Aprili, mwaka huu, hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema kama ambavyo Rais Kikwete alitumia sheria kutangaza upigaji kura hiyo, ni vema pia akafanya hivyo kuutengua kwa kuwa kuna udhaifu katika mchakato mzima.

Alisema zimebaki siku chache kufanyika mchakato huo, lakini hadi sasa elimu kuhusiana na suala hilo haijatolewa kwa wananchi.

“Kwa kuheshimu sheria, Rais ajitokeze atoe tangazo la kulifuta tangazo la serikali la kufanyika kwa kura ya maoni hadi baada ya uchaguzi mkuu. La sivyo, tutakwenda kubanana na udhaifu wa utendaji wake utaanikwa bungeni,” alisema Mnyika.

Alisema kabla ya mchakato huo, serikali ilipaswa kutoa elimu kwa umma miezi miwili na kutenga siku 30 kwa ajili ya kampeni, lakini vitu hivyo havijafanyika.

“Sheria inataka kuwe na uandikishaji, utoaji elimu, kampeni na uhakiki wa walioandikishwa katika daftari kama ni sahihi au umechakachuliwa, vitu ambavyo havijafanyika mpaka sasa,” alisema Mnyika.

Aliongeza: “Rais anakiuka sheria ya nchi kwa kulazimisha kura ya maoni kufanyika Aprili wakati bado kuna udhaifu mkubwa katika mchakato mzima wa zoezi hilo.”

Aliunga mkono kauli ya aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, aliyoitoa wakati akifanya mahojiano na NIPASHE juzi.

Jaji Warioba alisema kura ya maoni haiwezi kufanikiwa kutokana na maandalizi hafifu.

Alisema kwa mujibu wa sheria namba tatu ya mwaka 2014, ambayo inahusu kura ya maoni, jambo la kwanza linalotakiwa kufanyika ni uboreshaji wa daftari la wapigakura, elimu kwa umma kwa kipindi cha miezi miwili kisha kampeni za mwezi mmoja.

Aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kutangaza ratiba kamili ya kila eneo au uboreshaji wa daftari la wapigakura ndani ya wiki hii.

Alisema uboreshaji wa daftari hilo, ambao ulitakiwa kuwahi kwa ajili ya kufanikisha zoezi la upigaji kura ya maoni, lakini nalo limecheleweshwa kwa kuishia kuahirishwa mara kwa mara.

Wengine, ambao Mnyika alisema wataenda kubanwa bungeni kutokana na udhaifu wa utendaji wao katika kuchelewesha zoezi hilo, ni Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Wizara ya Fedha na Wizara ya Katiba na Sheria.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alipotafuta kuzungumzia kama amepokea taarifa ya Mnyika, alisema alikuwa katika kamati za Bunge zinazoendelea jijini Dar es Salaam, hivyo hakuwapo ofisini.

Alisema kama taarifa hiyo imepelekwa ofisini kwake anaamini imepokelewa na itafanyiwa kazi.

Rais Kikwete alitangaza zoezi la kura ya maoni Novemba 4, mwaka jana wakati akizungumza na wazee mjini Dodoma.

Alisema sheria ya kura ya maoni imeainisha muda wa wadau wa katiba kutoa elimu na kufanya kampeni, hivyo akataka sheria hiyo izingatiwe na kuheshimiwa ili kuepuka ugomvi.

Rais Kikwete alisema upigaji wa kura ya maoni kuhusu katiba hiyo utafanyika Aprili 30, baada ya elimu na kampeni juu ya kura hiyo kuanza rasmi Machi 30 na kuhitimishwa Aprili 29, mwaka huu kama sheria ya kura ya maoni inavyoelekeza.

Alisema imezoeleka kampeni ni siku 60, lakini baada ya kushauriana na wanasheria ilionekana siyo lazima isipokuwa inaamuliwa na rais kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment