HALI inazidi kuwa mbaya ndani ya Kambi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kufuatia taarifa za mgogoro mkubwa uliopo kati ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia.
Chanzo cha mgogoro huo ambao unafukuta, ni madai ya Slaa ya kutomwamini Mbatia anayedai ni pandikizi anayetumiwa na serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuvuruga umoja huo.
Inaelezwa, Slaa anamshutumu Mbatia kuwa ni Afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, hivyo ni hatari kwa ustawi wa umoja huo, na kuna uwezekano akasababisha kusambaratika kwake iwapo ataendelea kuwepo.
"Ukiwa nje huwezi kuona hali halisi ya mambo, kwa tulio ndani ndio tunaona kila kitu, huu umoja hauwezi kufika popote maana watu hawaamiani hata kidogo na kuna migogoro kila kukicha"
"Sasahivi Slaa anashinikiza Mbatia aondolewe UKAWA, anadai akiachwa atavuruga mpango wa kwenda ikulu" kilisema chanzo chetu kilichopo ndani ya kambi ya UKAWA.
Chanzo hicho kilisema, msimamo huo wa Slaa umewapa wakati mgumu vongozi wengine wa kambi hiyo na wanaona wakimtosa Mbatia watasababisha mgawanyiko wa wanachama, hivyo kuna uwezekano mkubwa wakampuuza Katibu Mkuu huyo.
"Slaa hapendi kumuona Mbatia akiwa UKAWA, ila Mbatia ni muhimu zaidi kuliko Slaa kwenye umoja huu maana anawakilisha chama na iwapo chama chake kitatoka kutasababisha mpasuko, kwahiyo kuna uwezekano mkubwa wakampuuza katibu mkuu, ila wakimpuuza unamjua mambo yake, ataanza vurugu ndani ya chama" kilisema chanzo chetu.
Aidha, mbunge mmoja wa CUF akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema, baadhi ya wanachama wa UKAWA wanamshutumu Mbatia kuwa mmoja wa walioshinikiza kambi hiyo kususia mchakato wa Katiba mpya na kushawishi wasirudi bungeni.
"Kuna mambo yanatia mashaka sana na leo viongozi wetu wanajuta, uamuzi wa kususia bunge la Katiba haukuwa sahihi, vongozi wetu walipotoshwa kususia bunge. Naamini kama tungebakia bungeni na kushindana kwa hoja, kingeeleweka"
"Mbatia alikuwa kinara wa kusisitiza tusirudi na kuna taarifa feki zilikuwa zinakuja ambazo zilionekana wazi mchakato ungekwama, lakini tumeona kilichotokea, CCM na baadhi ya wabunge wa UKAWA wakaendelea na wameandika walichotaka, na kwa hali ilivyo katiba wanayotaka wao itapita" alisema mbunge huyo kutoka Zanzibar (jina tunalihifadhi).
Mbunge huyo alisema, hali hiyo inaonyesha wazi kuna watu ndani ya kambi hiyo wanatumika na CCM, na mbinu ya kushawishi UKAWA wasirudi bungeni ilikuwa ni maagizo maalum yenye lengo la kuwapa nafasi CCM kupitisha mambo waliyotaka kwenye Katiba mpya.
Taarifa zaidi zinasema, jambo jingine ambalo linampotezea imani Mbatia kwa baadhi ya viongozi wenzake, ni uhusiano wake na kigogo mmoja mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ingawa mwenyewe mara kadhaa amekuwa akikana madai hayo na kushusha lawama kwa CCM kuhusika kusambaza madai hayo.
Inaelezwa, Mbatia amekuwa karibu na kigogo huyo na wamekuwa wakikutana mara kwa mara nyumbani kwake maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupeana maelekezo ambayo hawana shaka yanalenga kufanya hujuma kwa kambi hiyo.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na mwandishi wa habari hizi wamesema, kambi ya UKAWA ipo kwenye wakati mgumu ukiachilia mbali mgawanyiko uliopo katika suala la kuteua mgombea Urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, kuna hali ya kutoaminiana na kila mmoja anamuona mwenzake ni msaliti.
"Kabla hawajaungana Chadema waliwahi kukishutumu CUF kuwa ni tawi la CCM (CCM B), Wenje (Ezekiel Wenje) aliwahi kuwashutumu CUF kuwa ni chama cha mashoga, Chadema hao hao walishamuita Mbatia ni mbunge wa Rais Kikwete kwa kuwa aliteuliwa na Rais hivyo ni mbunge anayefuata maagizo ya CCM" alisema John Malingumu mchambuzi wa masuala ya kisiasa.
Mchambuzi huyo aliongeza kuwa, kila mmoja ndani ya kambi hiyo ameungana na mwenzake kwa malengo binafsi, ila hakuna mwenye imani na mwenzake.
"Pale kuna unafki mkubwa, kila mmoja amebaki na historia yake kichwani ya mambo ambayo walifanyiana kabla hawajaungana, utakumbuka pia Chadema waligoma kuunda Kambi ya Upinzani na CUF, haya yote hayajafutika"
No comments:
Post a Comment