Thursday, February 5, 2015

Tibaijuka, Muhongo wakosekana bungeni

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wameshindwa kuhudhuria vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma tangu vilipoanzia kutokana na sababu mbalimbali.
Profesa Muhongo alijiuzulu kutokana na maazimio ya Bunge ya kutaka awajibishwe kutokana na kashfa iliyoikumba wizara yake kutokana na sakata la uchotwaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow wakati Profesa Tibaijuka alivuliwa wadhifa wake akituhumiwa kupokea Sh1.6 bilioni zinazohusishwa na sakata hilo.
Mawaziri hao wa zamani ambao sasa wamebaki na nyadhifa zao za ubunge, hawajaonekana bungeni tangu mkutano wa 18 wa Bunge ulioanza wiki iliyopita.
Baada ya kujiuzulu, nafasi ya Profesa Muhongo ambaye ni mbunge wa kuteuliwa ilichukuliwa na George Simbachawene aliyewahi kuwa naibu wake wakati nafasi ya Profesa Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), imejazwa na William Lukuvi.
Katika maazimio yake, Bunge lilitaka viongozi wote waliohusika kwa namna moja au nyingine katika sakata hilo, mamlaka zao za uteuzi zitengue nafasi zao au wajiuzulu wenyewe.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema aliamua kujiuzulu baada ya kikao cha Bunge cha 16 na 17 akieleza kuwa ushauri wake kuhusu suala la escrow haukueleweka na ulichafua hali ya hewa. Pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yake.
Kwa nini hawaonekani?
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema jana kwamba Profesa Muhongo yupo safarini nje ya nchi na ndiyo maana hajaonekana bungeni, lakini ameomba ameomba ruhusa.
Kuhusu Profesa Tibaijuka alisema ni mgonjwa na ameomba ruhusa... "Hapa tunapozungumza Profesa Tibaijuka amenitumia meseji kuomba kuongeza siku saba nyingine kutokana na kuumwa."
Sakata la akaunti ya escrow
Suala hilo liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila na kusababisha mjadala mkali uliolilazimu Bunge kuipa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), jukumu la kuchunguza kashfa hiyo.
Baada ya kuwasilisha ripoti yake ya uchunguzi huo, katika mkutano wa Bunge uliomalizika mwishoni mwa Novemba mwaka jana, Bunge lilitoa maazimio manane, mojawapo likitaka kuwajibishwa kwa viongozi hao.Mwezi uliopita, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na mwenzake wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari walitishia kumtoa kwa mabavu bungeni Profesa Muhongo endapo bado angeendelea kushikilia wadhifa huo.
"Keshokutwa nakwenda bungeni kufanya kazi moja tu, nikimkuta Muhongo bungeni ndipo nitafukuzwa ubunge moja kwa moja," alisema Lema.CHANZO:MWANANCH

No comments:

Post a Comment