Thursday, January 8, 2015

TUMEBORESHA USAFIRI WA RELI YA KATI - MWAKYEMBE

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harisson Mwakyembe amesema watamaliza kipindi chao utawala wa awamu ya nne kwa kuimarisha usafiri wa Reli ya Kati uliokuwa 'umekufa' kwa muda mrefu.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo Dar es Salaam juzi usiku katika Kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV.
Alisema licha ya sekta ya reli kukabiliwa na changamoto mbalimbali, wizara yake imeendelea kuboresha sekta hiyo, ikiwamo kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wanaohujumu fedha za umma.
Dk Mwakyembe alisema tangu Serikali imtimue mwekezaji njia ya Reli ya Kati, ambayo ni Kampuni ya India ya Rites, mwelekeo uliopo ni kuhakikisha usafirishaji unaongezeka kwa tani za mizigo na abiria njia zote za reli nchini.(P.T)
"Kabla ya mwekezaji tulikuwa na uwezo wa kubeba tani milioni 1.5 na tulikuwa tunafikiria kwenda hadi tani milioni 5, lakini mwekezaji huyo alipoingia uzalishaji ukaanza kushuka tani 900,000 mara 500,000," alisema.
"Kinachosikitisha zaidi, mpaka tulifikia usafirishaji wa tani 190,000 kwa mwaka, tukaona hapana wacha atupishe ili tuanzishe harakati zetu wenyewe."
Dk Mwakyembe aliwaonya watumishi wabadhirifu, akisema hawatakuwa na nafasi ya kuendelea na ubadhirifu wao.
"Kwa mfano, udhaifu uliojitokeza kwenye ununuzi mabehewa, nasubiri uchunguzi wa kamati, hatuwezi kuwatuma watu kazi, halafu wanakwenda kupima suti India," alisema.
Kuhusu viwanja vya ndege, alisema kwa sasa wizara yake iko kwenye mpango wa kukarabati viwanja vikubwa vya ndege mikoani kabla ya kununua ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

No comments:

Post a Comment